Wakulima Sumbawanga wahimiza kilimo cha kisasa

0
1000

Baadhi ya wakulima mkoani Rukwa wameelezea umuhimu wa kuboresha miundombinu ya kilimo ili kuwawezesha kuendesha kilimo chenye tija kwa ajili ya ustawi wa jamii na shughuli za maendeleo.

Wakishiriki semina ya siku moja kuhusu matumizi ya teknolojia sahihi ya zana za kilimo iliyoandaliwa na Shirika la Taifa la Maendeleo – NDC wakulima hao wameshauri mtandao wa Benki ya Kilimo utumike kuwasaidia wakulima nchini.

Wamesema pamoja na ushauri wa wataalamu wa kilimo wanaopatikana katika maeneo mbalimbali nchini bado benki ya kilimo ina wajibu wa kuwawezesha wakulima katika jitihada zao za kuendesha kilimo cha kibiashara.

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi – CCM wilaya ya Sumbawanga Said King’eng’ena aliyekuwa mgeni rasmi kwenye semina elekezi hiyo amesema matumizi ya zana za kisasa za kilimo ikiwa ni pamoja na matrekta ni miongoni mwa mbinu sahihi za kuboresha kilimo.

Imeelezwa kuwa katika mpango wa kuwezesha kilimo chenye tija matreka 105 yatapelekwa mkoani Rukwa katika awamu ya kwanza ya maboresho ya kilimo kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo –NDC.