Wakulima Njombe watakiwa kutouza mazao kwa madalali

0
168

Mkuu wa mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka ametoa wito kwa wakulima mkoani humo kutouza mazao yao yakiwemo mahindi na mpunga kwa madalali na badala yake wakayauze kwenye vituo vya ununuzi vya halmashauri.

Amesema bei za madalali ni ndogo ukilinganisha na bei ya kwenye vituo vya ununuzi vya halmashauri.

Akizungumza katika mkutano wa kuhitimisha ziara ya Viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa mkoani Njombe, Mtaka amesema bei ya madalali inawanyonya sana wakulima kwa kununua mazao kwa bei ndogo na wao wanaenda kuuza kwa bei kubwa.

“Serikali kupitia NFRA tunanunua mahindi kwa shilingi 1,100, tunanunua mpunga kwa shilingi 800 kwa kilo, maana yake gunia la mahindi shilingi 110,000 serikali inanunua lakini pia tunanunua gunia la mpunga kwa shilingi 80,000. Hatuna sababu ya wakulima wa Njombe kuuza mahindi kwa madalali huko vijijini kwa bei ya hasara”. Amesema Mtaka na kuongeza kuwa

“Tumefungua vituo wilayani huko huko mnakotoa mahindi na mpunga. Niwaombe mkauze mahindi kwa bei ya soko, usimuuzie mtu mahindi kwa shilingi 40,000 akaenda kuuza 110,000 kwenye eneo ambalo ungefanyia usafirishaji 10,000 ukapeleka pale mahindi yako ukauza ukapata faida. Mtu ananunua mpunga 30,000 yeye anaenda kuuza 80,000”.