Wakazi wa Makete washirikiana kutatua changamoto zao

0
261

Wakazi wa vijiji vilivyopo katika kata ya Mang’oto wilayani Makete mkoani Njombe, wamefanya kazi ya kusafisha miundombinu katika chanzo cha maji iliyopo maeneo ya milimani.

Wakazi hao wametumia muda wa saa mbili kupanda milima hiyo ili kufika eneo yalipotegwa maji, eneo ambalo kwa takribani wiki sasa limeziba na kusababisha kukosekana kwa huduma ya maji kwa Wakazi wa kata hiyo ya Mang’oto.

Katika kufanya kazi hiyo ya kusafisha miundombinu ya chanzo cha maji, Wakazi hao wa kata ya Mang’oto wameshirikiana na Mbunge wa jimbo la Makete, – Festo Sanga .

“Nawashukuru Wananchi kwa kujitokeza kwa wingi, nimepanda mlima huu kwa tabu kweli na sehemu zingine ilinibidi niweke vituo vya kupumzika hadi nimefika, furaha yangu ni kujumuika nanyi kwenye kazi hii ambayo kwa leo imeleta matumaini ya kupatikana kwa maji, nawashukuru kwa uchaguzi, mmetuamini tushirikiane kwenye kuchapa kazi,” amesema Mbunge Sanga.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha wiki moja, kwa Mbunge huyo wa jimbo la Makete kufika kwenye kata hiyo ya Mang’oto, ambapo kwa mara ya kwanza alikwenda katika kijiji cha Ilindiwe kufunga vifaa vya umeme wa Sola katika zahanati ya kijiji hicho, ili zahanati hiyo iweze kutoa huduma za afya usiku na mchana.