Wakazi wa Kitunguru waonesha mfano wa kujikinga na corona

0
513
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kitunguru, Mwidini Mzee akimwaga maji ya kunawa mikono kwa kutumia mguu, ikiwa ni moja ya njia za kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Wakazi wa Kitongoji cha Kitunguru, Kijiji cha Kimbugu, wilayani Muleba, Kagera wamebuni utaratibu wa kunawa mikono ambapo wanatumia mguu kumwaga maji ili kuepuka kusambaa kwa virusi vya corona kwa kila mtu kushika kifaa chenye maji.

Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Mwidini Mzee ameliambia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuwa wamebuni utaratibu huo ili kupunguza gharama kwa wakazi kununua ndoo za kuwekea maji.

Mwidini ameongeza kuwa kwa sasa kila kaya ina kifaa hicho na wakazi wengi wamehamasika kufuata taratibu zinazoelekezwa na watalam wa afya kuhusu namna ya kuepuka maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha homa ya mapafu (COVID-19).

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Justo Rwabunywege amesema zoezi linaloendelea kwa sasa ni kushirikiana na watalam wa afya kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala mbalimbali kuhusu COVID-19.