Wakazi wa Ipelele kupata chanzo kingine cha maji

0
186

Wataalam wa Maji kutoka Idara ya Maji wilayani Makete mkoani Njombe kwa kushirikiana na Jumuiya ya Watumiaji Maji ya kata ya Ipelele, wanaangalia uwezekano wa kuongeza chanzo kingine cha maji ili kumaliza tatizo la maji kwenye kata hiyo.

Hatua hiyo inafuatia ombi la Mbunge wa jimbo la Makete, -Festo Sanga na baadhi ya Wakazi wa kata hiyo ya Ipelele, kutokana na kata hiyo kuwa na tatizo la kukosekana kwa maji safi na salama kwa muda mrefu.

Wakiwa kwenye safu za uwanda wa Mbuga ya Kitulo, Sanga amewaomba Wataalam hao wa Idara Maji kupima usalama wa maji wanayotumia Wananchi wa Ipelele baada ya wananchi hao kudai kuwa yanachanganyika na yale yanayotoka barabarani na kukifanyia ukarabati chanzo cha zamani cha maji ikiwa ni pamoja na kuweka fensi na nyavu ili kuzuia wadudu waisiingie kwenye bomba la maji.

Uongozi wa Idara ya Maji wilayani Makete umesema unayafanyia kazi maombi hayo, na kwamba ukarabati wa chanzo cha zamani cha maji utakamilika katikati ya mwezi Februari mwaka huu.

Baadhi ya Wakazi wa kata ya Ipelele wamewashauri Watumishi wa Serikali kufanya kazi kwa kasi ya Rais John Magufuli na wasisubiri malalamiko ya Wananchi ndipo watatue kero zao.

Wamesema tatizo la kukosekana kwa maji safi na salama katika kata yao ni la muda mrefu, hivyo wanaomba wapatiwe chanzo kingine cha maji ambacho tayari wao wenyewe wamekibaini kwenye maeneo ya milimani.