Msajili Mkuu Bodi ya Usajili wa Makandarasi Mhandisi Rhoben Nkori amewataka wakandarasi nchini kuwa makini wakati wa kuandaa zabuni kwa kuwatafuta wataalam wa miradi waaminifu na wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha ili kuepuka kwenda kinyume na matakwa ya miradi wanayoomba.
Mhandisi Nkori ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wa kuandaa zabuni wakandarasi wa mikoa ya nyanda za juu kusini ambapo amesema wakandarasi wengi wameshindwa kukamilisha miradi kwa wakati kutokana na kukosa taarifa sahihi za uhalisia wa miradi wakati wa awali.
Kwa upande wao baadhi ya wakandarasi wameomba kutatuliwa baadhi ya changamoto zao zikiwemo usawa wa kijinsia, mikopo ya vifaa na makato ya Mamlaka ya Mapato TRA.
Mafunzo hayo yamefanyika kufuatia kuongezeka kwa matumizi ya mfumo mpya wa majenzi ya serikali ya kutumia wataalam wa ndani Force Account hali inayokosesha miradi wakandarasi wa sekta binafsi pamoja na uwepo wa mfumo mpya wa matumizi ya kieletroniki wa maombi ya Zabuni.