Jeshi la Polisi mkoani Arusha limefanikiwa kukamata watu wawili kwa tuhuma ya kukutwa na Nyama Pori ya mnyama pofu kwa Kilogram 150.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha ACP. Justine Masejo amesema kuwa tarehe 02.03.2022 muda wa 07:30 mchana huko maeneo ya Ngarenaro katika Halmashauri ya jiji la Arusha askari Polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili ambao ni Amanda Thomas (22) mkazi wa kwa Morombo na Kelvin Thomas (27) mkazi wa Ngarenaro.
Masejo amesema kuwa uchunguzi wa awali wa tukio hili umebaini kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo ya nyara za serikali ambapo uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na askari wanyama Pori ili kubaini mtandao wao.
Ameendelea kusema kuwa katika tukio jingine tarehe 02.03.2022 muda wa saa 09:30 alasiri huko kata ya Rhotia tarafa ya mbulumbulu wilaya ya Karatu na mkoa wa Arusha askari Polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili ambao ni Petro Gaudence (57) mkazi wa mbulumbulu na Revocatus Protus (28) mkazi wa mbulumbulu wakiwa na lita 570 za Pombe haramu ya moshi (gongo).
ACP Masejo amewambia waandishi kuwa Operesheni kali inaendelea katika wilaya zote ilikubaini wanaofanya biashara hizo haramu, hivyo ametia wito kwa wanaojihusisha na biashara hizo kuacha na kusisitiza kuwa Jeshi la polisi halitomfumbia macho mtu yeyote anayejihusisha na biashara haramu.