Wakamatwa kwa kusafirisha vinyonga na nyoka nje ya nchi

0
179


 
Wizara ya Maliasili na Utalii imewakamata Watanzania wanne wanaotuhumiwa kusafirisha vinyonga hai 74 na nyoka sita kinyume cha sheria, na kuwauzia raia wawili wa Czech.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro amesema kuwa, vinyonga na nyoka hao walikamatwa Januari 22 mwaka huu nchini Austria na kuhifadhiwa katika hifadhi ndogo ya wanyama nchini humo.

Watuhumiwa hao  wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hapo kesho, wakikabiliwa  na makosa ya kusafirisha nje wanyamapori hao bila kibali, uhujumu uchumi pamoja na utakatishaji fedha kupitia biashara hiyo.

Dkt Ndumbaro amesema vinyonga na nyoka hao wanaodaiwa kutoka katika milima ya Usambara, walikamatwa na maafisa wa forodha wa Austria wakiwa kwenye begi ambalo ndani yake waliwekwa kwenye soksi na kuingizwa kwenye vifungashio vya plastiki.

Amesema uchunguzi unaendelea katika maeneo mbalimbali, ili kubaini namna vinyonga na nyoka hao walivyopitishwa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mkoani Dar es salaam bila kugundulika. 

Mwezi Mei mwaka 2016, Serikali ilisitisha usafirishaji wa Wanyamapori hai kwenda nje ya nchi, ili kuwalinda Wanyapori hao na kukuza sekta ya utalii nchini.