Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Mabula Mchembe ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kufuatilia matumizi ya vitambulisho vya wakaguzi wa mamlaka hiyo ili kubaini wanaovighushi kwa nia ya kujipatia rushwa.
Prof. Mchembe ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa vitambulisho 524 vya wakaguzi vilivyoboreshwa hafla iliyofanyika katika ofisi za TMDA jijini Mwanza.
Amesema mamlaka hiyo ina jukumu la kufuatilia vitambulisho vya wakaguzi ili kumlinda mwananchi kwa kuhakikisha bidhaa zinaendelea kuwa bora na salama kwa matumizi ya binadamu.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo amesema uwepo wa vitambulisho vilivyoboreshwa utatatua changamoto ya kujitokeza kwa watu wasio waaminifu ambao wamekuwa wakitengeneza vitambulisho bandia kwa nia ya kuwalaghai wananchi.