Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson amelitaka Baraza la Amani na Usalama la Wabunge wa nchi za Maziwa Makuu (FP-ICGLR) kujadili kwa kina masuala yanayochochea migogoro katika nchi zao na kupendekeza namna ya kuyapatia ufumbuzi.
Dkt Tulia ametoa kauli hiyo jijini Arusha wakati akifungua kikao cha Tano cha Baraza hilo na kuongeza kuwa migogoro ya mara kwa mara katika nchi za Maziwa Makuu imekuwa ikiathiri uchumi, hivyo ni vema Wabunge waliopewa dhamana na nchi zao kutafuta njia za kuiepuka.
Amewaambia wajumbe wa Baraza hilo la Amani na Usalama la Wabunge wa nchi za Maziwa Makuu kutoka nchi 12 za Afrika kuwa, baraza hilo ni moja ya vyombo muhimu katika nchi za Maziwa Makuu vyenye jukumu la kuimarisha amani na usalama.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa FP-ICGLR Balozi Onyango Kakoba amesema kuwa wakati wa kikao chao wanadajili masuala mbalimbali yakiwemo yale ya kisera yanayoweza kuchangia kuhamasisha amani katika nchi za Maziwa Makuu.
Mmoja wa Wajumbe wa Baraza hilo la Amani na Usalama la Wabunge wa nchi za Maziwa Makuu kutoka Tanzania Dkt Christine Ishengoma amesema kuwa baada ya kikao hicho muhimu wanatarajia kutoa mapendekezo yatakayoonesha njia za kuboresha hali ya amani na usalama.