Wajasiriamali Kigamboni wapokea mikopo ya kujiendeleza

0
392

Mbunge wa Kigamboni amegawa mikopo yenye thamani ya TSh 130 millioni kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu vya Wilaya ya Kigamboni katika sherehe iliyofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Kigamboni.

Dkt Faustine Ndugulile ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kwa kutenga na kutoa mikopo kwa wajasiriamali ambapo hadi sasa imetoa TSh 1.25 billioni tangu kuanzishwa kwake miaka minne iliyopita.

Dkt Ndugulile amewataka waliopewa mikopo kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha fedha hizo kwa wakati.

Aidha, amewapongeza maofisa maendeleo ya jamii kwa kazi nzuri ya uhamasishaji na kusimamia vikundi hivyo, huku akiwataka kuiga mfano wa Ludewa ambako vikundi vya wajasiriamali vimewezeshwa kupata kandarasi mbalimbali za barabara kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).