Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (Mahakama ya Mafisadi), imewahukumu kifungo cha maisha jela Abdul Nsembo na mkewe Shamim Mwasha baada ya kutiwa hatiani kwa kosa ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin.
Aidha, mahakama hiyo imetoa amri ya kutaifisha mali za wawili hao, ikiwemo gari aina ya Discover 4 na dawa hizo zimetakiwa kuteketezwa.
Wawili hao walikamatwa Mei 1, 2019, eneo la Mbezi Beach mkoani Dar es Salaam wakiwa na gramu 232.70 za dawa za kulevya aina ya heroin na kufunguliwa shauri la uhujumu uchumi namba 36 la mwaka 2019.
Katika maelezo yaliyosomwa mbele ya mahakama wakati kesi hiyo ikiendelea, upande wa mashitaka ulidai kwamba mshitakiwa wa kwanza Abdul Nsembo anatuhumiwa kufadhili biashara ya dawa za kulevya kwa muda mrefu huku akiwa na mtandao mkubwa ndani na nje ya nchi.