Wagonjwa 45 kufanyiwa upasuaji wa moyo

0
890

Jumla ya wagonjwa 45 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo wa bila kufungua  kifua katika kambi maalum ya matibabu ya moyo kuanzia Tarehe 7 hadi 18 mwezi huu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete       -JKCI.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Uhusiano cha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete imesema kuwa upasuaji huo unafanywa  kupitia madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa kushirikiana na Madaktari Afrika na Shirika la Cardio Start wote kutoka nchini Marekani.

Matibabu yanayofanyika  katika kambi hiyo ni upasuaji wa kufungua kifua bila kufungua kifua ambao unafanyika kupitia tundu dogo kwenye paja kwa wagonjwa kuzibuliwa mishipa ya moyo iliyoziba yaani                  -Percutaneous Coronary Intervention na kuwekewa vifaa  vinavyosaidia kurekebisha mapigo ya moyo ambavyo ni Permanent Pacemaker na High Powered Devices.

Wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji ni wale wenye matatizo ya moyo ambayo ni valve, mishipa ya moyo iliyoziba, moyo kushindwa kufanya kazi vizuri, matibabu kwa watu wazima waliozaliwa na matatizo ya moyo na wale wenye matatizo ya moyo yaliyotokana  na ugonjwa wa Kisukari.

Kambi hii inaenda  sambamba na utoaji wa elimu kwa madaktari na wauguzi pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi kwa wageni na wataalamu kutoka nchini Marekani.

Hii ni kambi ya kwanza ya matibabu ya moyo tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2019 na ni mara ya kwanza kwa Shirika Cardio Start  kuja hapa nchini.