Wagonjwa 15 kuzibuliwa mishipa ya damu JKCI

0
379

Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es salaam kwa kushirikiana na wenzao wa  hospitali ya Meditrina ya nchini India,  wanafanya kambi maalumu ya matibabu ya moyo ya kuzibua mishipa ya damu kwa wagonjwa ambao mishipa yao imeziba kwa kiwango kikubwa (Chronic Total Occlusion) na hivyo kushindwa kupitisha damu vizuri.

Kambi hiyo ya muda wa siku tatu, ni maalum kwa ajili ya  kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo hayo,  ambao bila ya kupata mtaalamu mwenye ujuzi wa hali ya juu wa kuzibua mishipa hiyo,  wangefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo.

Matibabu hayo yanafanyika kwa kutumia mtambo wa Cathlab,  ambapo mgonjwa anatobolewa tundu dogo katika paja ambalo linapitishwa vifaa maalum vya kuzibua mishipa ya damu ya moyo (Stent).

Katika kambi hiyo,  wataalamu wa afya wa JKCI watapata elimu ya jinsi ya kuzibua mishipa ya damu ya moyo ambayo imeziba kwa kiwango kikubwa.

Jumla ya wagonjwa 15 ambao mishipa yao ya damu mmoja hadi mitatu imeziba,  wanatatibiwa katika kambi hiyo iliyoanza leo tarehe 23 hadi  tarehe 25 mwezi huu.