Wagoma kuuza korosho mnadani

0
241

Wakulima wa korosho wa wilaya za Tandahimba na Newala mkoani Mtwara wamegoma kuuza korosho zao ambazo ni zaidi ya tani 1,600 kwa bei ya juu ya shilingi 2,011 kwa kilo na bei ya chini ya shilingi 1,630 kwa kilo, kwa madai kuwa bei hiyo ni ndogo na haina faida kwao.

Wakulima hao wamefikia uamuzi huo wakati wa mnada wa kwanza wa uuzaji korosho kwa msimu wa mwaka huu uliofanyika katika kijiji cha Mitondi B wilaya ya Tandahimba.

Wamesema bei ambayo imepangwa kwa ajili ya kuuza korosho ni ndogo na kusema wanataka kuuza korosho hizo kati ya shilingi 2, 500 na elfu tatu kwa kila kilo moja ya korosho.

Wakulima hao wa korosho wa wilaya za Tandahimba na Newala wamegoma kuuza korosho hizo mbele ya mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas, ambaye ndiye aliyezindua mnada wa kwanza wa uuzaji korosho kwa msimu wa mwaka huu mkoani humo.

Katika uzinduzi huo Kanali Abbas aliongozan na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Mtwara, wakuu wa wilaya, viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika na viongozi wa vyama vikuu pamoja na viongozi kutoka Bodi ya Korosho Tanzania (CBT).