Katika kuadhimisha miaka 55 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rais John Magufuli kwa kutumia madaraka aliyopewa, ametoa msamaha kwa wafungwa 3,530.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeonesha kuwa kati ya wafungwa hao 3,530 waliopatiwa msamaha, wafungwa 722 wataachiwa huru hii leo na wafungwa wengine 2,808 watabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huo.
Miongoni mwa wafungwa waliopatiwa msamaha huo ni wale wenye magonjwa kama Ukimwi, Kifua kikuu na Saratani ambao wako kwenye hatua mbaya ya ugonjwa huo.
Wafungwa wengine walionufaika na msamaha huo ni wale Wazee wenye umri wa miaka sabini au zaidi, Wafungwa wa kike walioingia na ujauzito gerezani, Wafungwa walioingia gerezani na watoto wanaonyonya na wasionyonya na Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa msamaha huo wa Rais katika kuadhimisha miaka 55 ya Muungano hautawahusu wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa au kwa makosa ya kujaribu kuua, kujaribu kujiua au kuua watoto wachanga na Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.
Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya, Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa na Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo hawahusiki na msamaha huo.