Wafugaji kunufaika na mbegu bora za mifungo ya asili

0
235

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ametoa wito kwa wafugaji wa mifugo ya asili kuunga mkono mkakati wa uboreshaji kosaafu za mifugo nchini ili kupata tija zaidi kwa taifa kwa kuwa koo za mifugo zinazopatikana hapa nchini ni nzuri.

Waziri Ndaki amebainisha hayo jijini Dodoma, wakati akizindua mpango mkakati wa uboreshaji kosaafu za mifugo nchini wenye lengo la kuhakikisha kosaafu hizo zinazopatikana katika Bara la Afrika na maeneo mengine duniani, zinahifadhiwa na kudumishwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi na raia wake.

“Ilikuwa lazima mkakati uzinduliwe leo kuhakikisha yale yaliyosemwa kwenye Sera ya Mifugo mwaka 2006, sasa yanakamilishwa kwa sababu tunaweza kuboresha kosaafu ya mifugo lakini hatukuwa na mikakati ya namna sera hiyo inaweza kuboresha kosaafu ya mifugo yetu ya asili,” amesema Waziri Ndaki

Aidha Waziri Ndaki amesema hapa nchini kuna mifugo ya aina nyingi na hizo zote ni kosaafu za mifugo ambazo zinatakiwa kulindwa kuhifadhiwa na kuendelezwa, kwa njia ya ubora zaidi ili kunufaisha watu wake hivyo mkakati huo utasaidia kuona namna gani ya kuboresha ili ziweze kuwanufaisha zaidi wafugaji.

Kwa upande wake Mratibu wa Kosaafu za Mifugo hapa nchini kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Hassan Mruttu amesema tayari kulishakuwa na rasimu na kuanza utekelezaji kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Afrika la Rasilimali za Mifugo (AU-IBAR) kwa kuanzisha kikundi cha wafugaji wa mbuzi weupe wa kipare na kuwezesha kupata mbegu ya ng’ombe aina ya sahiwal, ambayo inakuwa na nyama na maziwa mengi pamoja na kusaidia uhifadhi wa mbegu hizo.