Wafikwa na umauti wakigombea mwanamke.

0
197

Vijana wawili Ibrahimu Shaban (21) na Mussa Bakari (28) wamefariki dunia wilayani Masasi mkoani Mtwara, baada ya kupigana magongo wakati wakigombea mwanamke aliyefahamika kwa jina la Hadija Msamati.

Kaimu Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo amesema tukio hilo limetokea tarehe 29 mwezi huu majira ya saa sita usiku katika kijiji cha Mkangaula kata ya Namalenga wilayani Masasi.

Amesema tukio hilo limesababishwa na wivu wa mapenzi na baada ya kufanyika kwa uchunguzi Jeshi la Polisi limebaini marehemu hao walikuwa kwenye ugomvi wa kugombea mwanamke ambaye baada ya tukio hilo alitoweka na kwenda pasipojulikana.

Miili ya marehemu hao imefanyiwa uchunguzi na kubainika kuwa chanzo cha vifo hivyo ni kuvuja damu kwa wingi mwilini.

Jeshi la Polisi mkoani Mtwara linaendelea na juhudi za kumsaka mwanamke huyo kwa ajili ya mahojiano zaidi.