Naibu Waziri wa Viwanda, Exaud Kigahe amewataka wafanyabiashara na walaji kuwasilisha malalamiko Tume ya Ushindani (FCC) mara wanapobaini wameuziwa bidhaa bandia.
Kigahe alisema hayo alipokuwa akijumuisha maoni na mapendekezo ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira wakati wa semina iliyolenga kuwaelimisha wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Ushindani na mafanikio yake iliyofanyika Agosti 31, 2021 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Alisema wafanyabiashara na walaji wanapaswa kutumia FCC kufikisha malalamiko pindi wanapouzia bidhaa bandia Ili tatizo hilo lishughulikiwe kwa haraka.
Aidha, Naibu waziri Kigahe ametumia fursa hiyo kuiagiza FCC kuongeza kasi ya kushughulikia malalamiko yanayowasilishwa na kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wafanyabiashara na walaji kuhusu hatua za kufuata katika uwasilishaji wa malalamiko mara wanapoona au kuuziwa bidhaa bandia na jinsi ya kuzitambua bidhaa hizo.
“FCC wanatakiwa kukagua bidhaa bandia hususani zile zenye madhara kwa maisha ya binadamu kila mara pamoja na kujipanga kukagua bidhaa bandia zinazouzwa kwa njia ya mtandao” Amesema Kigahe.
Nao, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira wametoa maoni na mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha huduma zinazotolewa na FCC hususani katika kusimamia ushindani wa haki katika Biashara zote ikiwemo ujenzi wa barabara pamoja na bidhaa zinazozalishwa na wajasiliamali wadogo.
Akiwaelimisha Wajumbe wa Kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani William Erio amesema kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani (Na. 8) ya Mwaka 2003, FCC inajukumu la kukuza ustawi wa Watanzania kwa kushajiisha (promote) na kulinda ushindani wa kibiashara na kumlinda mlaji dhidi ya mienendo kandamizi na hadaifu katika soko la Tanzania Bara.
Amesema katika udhibiti wa bidha bandia, kuanzia mwaka 2018 hadi 2021, FCC imefanya ukaguzi katika Bandari ya Dar es Salaam na Bandari Kavu DSM ambapo makasha ya kusafirishia mizigo 1,699 yalikaguliwa na makasha 545 yalibainika kuwa na baadhi ya bidhaa zilikuwa na nembo za bidhaa halisi huku zikinge zikiwa hazionyeshi nchi na mahali bidhaa zilipotengenezwa