Wafanyabiashara wanne wa madini wahukumiwa

0
354

Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza imewahukumu wafanyabiashara wanne wa madini ya dhahabu kwa pamoja kutumikia kifungo cha miaka 38 jela au kulipa faini ya shilingi milioni 529.8 baada ya kukiri makosa 9 yakiwemo ya uhujumu uchumi, rushwa pamoja na utakatishaji wa fedha yaliyokuwa yanawakabili.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Mwanza Rhoda Ngimilanga baada ya watuhumiwa hao Sajid Abdalah, Kisabo Nkinda, Emmanuel Kija na Hassan Sadick kukiri makosa yaliyokuwa yanawakabili.

Aidha watuhumiwa wengine wanane ambao ni askari polisi wamekana mashtaka yanayowakabili na wamerejeshwa rumande hadi April 10 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Kesi hiyo namba 3 ya mwaka 2019 ilianza kusikilizwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza baada ya upande wa jamhuri kuwasilisha hati mpya ya mashtaka.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo iliyodumu kwa zaidi ya saa saba washtakiwa namba moja hadi namba nne ambao ni wafanyabiashara wa madini walikiri mashtaka yanayowakabili huku washtakiwa namba tano hadi kumi na mbili ambao ni maofisa wa polisi wakikana makosa.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili Castus Ndamugoba uliwasilisha vielelezo kadhaa mbele ya Hakimu mMawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Mwanza Rhoda Ngimlanga vikiwemo fedha kiasi cha shilingi milioni mia saba, kilo 319.59 za madini ya dhahabu zenye thamani ya shilingi bilioni 27.

Vielelezo vingine vilivyowasilishwa mahakamani hapo ni hati za upekuzi na za kukamata mali, magari mawili, mashine ya kupimia dhahabu ambavyo vilitambuliwa na washtakiwa namba moja hadi namba nne.

Kufuatia washtakiwa wa kwanza hadi wa nne kukiri mashtaka yaliyokuwa yanawakabili,hakimu mfawidhi Ngimilanga amewahukumu kutumikia kifungo cha miaka 38 jela au kulipa faini ya millioni 202 wote kwa pamoja huku washtakiwa wa tano hadi 12 ambao ni askari polisi wakirejeshwa rumande baada ya kukana mashtaka dhidi yao.

Inadaiwa kuwa tarehe nne Januari mwaka huu watuhumiwa Sajid Abdalah, Kisabo Nkinda, Emmanuel Kija na Hassan Sadick waliwapatia watuhumiwa wanane ambao ni askari polisi rushwa ya Shilingi Milioni mia saba ili kuwasaidia kutorosha Kilo 319 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Billioni 27.

Watuhumiwa hao ambao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Tarehe 11 mwezi Januari mwaka huu walikamatwa wilayani Sengerema Mkoani Mwanza Januari nne mwaka huu wakidaiwa kushiriki mpango wa kutorosha Kilo 319 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Billioni 27.