Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya kushirikiana na si kushindana, ili uchumi wa mataifa hayo uendelee kukua.
Rais Samia Suluhu hassan ambaye yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Kenya, ametoa wito huo wakati wa mkutano wa jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya uliofanyika jijini Nairobi.
Amesema hatua ya Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya kuingia kwenye ushindani usio na tija hauwezi kuwa na matokeo chanya, na kwamba ushirikiano kati yao ndio jambo muhimu.
Amesisitiza kuwa Tanzania ipo tayari kuwapokea Wafanyabiashara kutoka Kenya na pia ipo tayari kuwa daraja katika kuhakikisha biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili unafanikiwa.
Mkutano huo wa jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya ulikuwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu fursa za biashara na uwekezaji zilizopo katika nchi hizo mbili.