Rais Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano kati ya chemba ya biashara ya Tanzania, Zanzibar na chemba ya biashara ya Qatar.
Kwa upande wa chemba ya biashara ya Tanzania, mkataba huo umesainiwa na Rais wa chemba hiyo Paul Koyi, huku Zanzibar ukisainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC) Ali Suleiman Amour.
Kwa upande wa Qatar mkataba huo umesainiwa na Makamu Mwenyekiti wa chemba ya biashara ya nchi hiyo Muhammed Bin Ahmed Al Kuwari.
Lengo la mkataba huo uliosainiwa huko DOHA, ni kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Qatar hasa kwenye sekta za utalii, miundombinu, ujenzi wa hoteli na usambazaji wa gesi.
Mbali na kushuhudia utiaji saini mkataba huo, Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Waziri wa Fedha wa Qatar, Ali bin Ahmed Al-Kuwari ambapo wamejadili masuala ya kikodi baina ya nchi hizo mbili, uwekezaji, biashara, gesi, ufugaji, utalii na kilimo.
Na katika mazungumzo yake na Waziri wa Afya wa Qatar, Dkt. Hanan Mohamed Al Kuwari wamekubaliana wataalamu wa Tanzania wabadilishane uzoefu kwenye sekta ya afya hasa katika huduma za kibingwa na za dharura.
Rais Samia pia katika ziara yake ya kikazi amefanya mazungumzo na Amiri wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al Thani, wafanyabiashara wakubwa na kuhudhuria mkutano wa ubunifu wa Afya Duniani (World Innovation Summit for Health) uliomalizika hii leo.