Wafanyabiashara Mtwara waungana na wenzao kugoma

0
247

Wafanyabishara wa Soko Kuu la Mtwara, Soko la Mkanaledi na maeneo ya Skoya Manispaa ya Mtwara – Mikindani wamefunga maduka yao kwa madai kuwa uongozi wa Manispaa ya Mtwara – Mikindani umefunga baadhi ya maduka kwa kuweka utepe ili kuwashinikiza kulipa kodi.

Wakizungumza sokoni hapo baadhi ya wafanyabiashara hao wamesema Juni 25, 2024 uongozi wa manispaa ulifika katika soko hilo na kufunga baadhi ya maduka bila kutoa taarifa kwa wenye maduka wala uongozi wa soko hilo.

Aidha, wafanyabiashara hao wameongeza kuwa kodi za mabanda zimepanda katika soko hilo wakitolea mfano mabanda ya bati kodi imepanda kutoka shilingi elfu 15 hadi shilingi elfu 40.

Mabanda madogo ya tofali yamepanda kutoka shilingi elfu 45 hadi shilingi elfu 75 na mabanda makubwa yamepanda kutoka shilingi elfu 75 hadi shilingi laki moja.

Mwenyekiti wa Soko Kuu la Mtwara, Msham Kaisi amekiri kufungwa kwa maduka yote katika soko hilo na uongozi wa manispaa pasipo kutoa taarifa kwa wafanyabiashara na uongozi wa soko, jambo ambalo amesema si la kiungwana.

Tayari uongozi wa mkoa, uongozi wa manispaa, chama cha wafanyabiashara  na uongozi wa soko hilo wamekutana kwa ajili ya kujadili changamoto hiyo ili kutoka na jibu la moja la kuondoa hali hiyo.