Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kulinda mazingira, yakiwemo mazingira ya bahari.
Hatua hizo ni pamoja na kupiga marufuku utumiaji wa mifuko ya plastiki inayotumika mara moja, kutenga asilimia 6.5 eneo la bahari ya Hindi kuwa eneo tengefu la bahari na kudhibiti kwa asilimia 99 uvuvi haramu.
Hayo yameelezwa mkoani Dar es Salaam na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango
wakati akifungua warsha ya Umoja wa Mataifa kuhusu tathmini, usimamizi na utunzaji wa mazingira ya bahari.
Amewaeleza washiriki wa warsha hiyo kuwa, ushirikiano baina ya mataifa pamoja na kujitolea ni mambo muhimu yatakayosaidia matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na kuepusha kupotea kwa rasilimali hizo.
Amesema ni lazima kuzuia na kupunguza uchafuzi wa bahari kwa kila namna kuanzia vyanzo vya ardhini hadi baharini.
Kwa mujibu wa Dkt. Mpango, kwa sasa katika kulinda bahari vinahitajika vitendo zaidi vitakavyokwenda pamoja na sayansi, uvumbuzi na teknolojia na ushirikishwaji wa wadau wote.