Wabunge watofautiana kuhusu takwimu za uchumi wa Tanzania

0
217

Mkanganyiko umeibuka bungeni baada ya taarifa za wabunge ambao ni wanazuoni kutofautiana kuhusu kundi ambalo Tanzania ipo, kati ya uchumi wa kati daraja la chini au kundi la nchi masikini.

Sintofahamu hiyo imetokana na taarifa za Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo na Mbunge wa Ubungo Profesa Kitila Mkumbo kutofautiana.

Kwa upande wake Profesa Muhongo amesema kuwa Tanzania imeshuka kutoka kundi la nchi zenye uchumi wa kati, daraja la chini, kwenda kundi la nchi masikini.

“GDP per capita [Pato la Taifa gawanya kwa idadi ya watu] inakadiriwa mwishoni mwa mwaka itakuwa dola za Marekani 990. Kwa maneno mengine tumerudi chini, tutaenda kwenye kundi la nchi masikini kufuatana na viwango vilivyowekwa na Benki ya Dunia (WB) tarehe 1/7/2021.” amesema Profesa Muhongo

Licha ya taarifa hiyo, Mbunge wa Ubungo Profesa Kitila Mkumbo ameitaka wizara ya Fedha na Mipango kuweka wazi kundi ambalo Tanzania ipo kwa sababu kwa taarifa alizosoma leo, Tanzania bado ipo uchumi wa kati.

“Nchi yetu mwaka 2021 ilikadiriwa kuwa na pato la dola za Marekani bilioni 67.78 na sio bilioni 62 [alizotaja Prof. Muhongo]. Ukifanya hesabu kwa idadi ya watu ya sasa inatupa DGP per capita income ya dola za kimarekani 1,135.5 [tofauti na dola 990 alizotoa Prof. Muhongo].” amesema Profesa Mkumbo

Ameongeza kuwa hoja kwamba Tanzania imetoka uchumi wa kati haiwezi kuwa ya kweli na kwamba “ni muhimu tukalinda mafanikio yetu kwa wivu mkubwa sana. Kwa hiyo ningeomba Waziri wa Fedha atakapohitimisha hili jambo atolee kauli nzito ya kueleweka ili nchi isibabaike, tumeshuka au tumepanda.”

Katika mwaka 2021, pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 4.9 ikilinganishwa na asilimia 4.8 mwaka 2020.

Aidha, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2022 (Januari hadi Juni), uchumi ulikua kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2021.