Serikali imesema imepokea maoni ya wabunge kuhusu changamoto ya wingi wa waombaji wa ajira dhidi ya nafasi zilizotangazwa na inaifanyia kazi ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu.
Ahadi hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Ritta Kabati ambaye alitaka kufahamu kwanini Serikali isiangalie vigezo na kuepusha kuwaita waombaji wengi.
“Tunapotangaza matangazo matarajio yetu ni kwamba watajitokeza wengi ili waje kushindana kwa ajili ya kupata nafasi hizi,” amesema naibu waziri huku akisisitiza kwamba watakapokamilisha utaratibu mpya watatoa taarifa.
Aidha, akijibu swali la Mbunge Rashid Shangazi kuhusu wakazi wa vijijini kupata taarifa za ajira, Naibu waziri amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha kuwa matangazo yote ya ajira yanakwenda hadi ofisi za kata na vijiji ili kumwezesha kila Mtanzania kupata fursa ya kuomba nafasi hizo na kuleta ushindani wa haki.
Kwa upande wake Mbunge wa Liwale, Zuberi Chauka amehoji kuwa Serikali haioni haja sasa ya kuwapa posho wale wanaoitwa kwenye usaili jijini Dodoma ili waweze kujikimu muda wote watakaokuwepo huko.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri amesema hilo ni suala la kibajeti na kisera hivyo Serikali itakapokuwa imejenga uwezo italifanyia kazi lakini kwa sasa ni jambo gumu.
Ameongeza kuwa Serikali inaufanyia kazi mfumo mzima wa ajira ili kutatua changamoto zinazojitokeza.