Wabunge wa Uganda watembelea TCRA kujifunza

0
175

Wabunge kutoka Uganda na maofisa wa masuala ya Teknolojia ya Haabari na Mawasiliono (TEHAMA) wa nchi hiyo wametembelea Ofisi Kuu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kujifunza jinsi Tanzania inavyosimamia sekta ya mawasiliano yanayohusisha mawasiliano ya simu, intaneti, utangazaji na huduma za posta.

Wabunge waliokuja nchini ni wa Kamati ya Bunge la nchi hiyo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) pamoja na Miongozo ya Kitaifa wakiwa wameandamana na maofisa wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Uganda (NITA-U),

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Tony Ayoo, wabunge hao, leo Machi 27, 2024 wamepata fursa ya kuelezwa kwa kina jinsi TCRA inavyohudumia wadau mbalimbali katika sekta ya mawasiliano, ikiwemo wamiliki wa leseni, watumiaji wa huduma za mawasiliano na wadau wa sekta ya umma.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, John Daffa, aliwakaribisha wabunge hao na kuwapitisha katika maelezo kuhusu majukumu ya TCRA na mchango wake katika kusimamia mawasiliano.

“Jukumu letu ni kuhakikisha kwamba huduma zote zinazohusu mawasiliano, zilizo ndani ya ikolojia ya teknolojia ya habari na mawasiliano, zinasimamiwa kwa ufanisi ili zichangie maendeleo ya nchi yetu,” amefafanua Daffa.

Kamati hiyo pia imejifunza kuhusu namna TCRA inavyotekeleza majukumu yake ya kusimamia rasilimali muhimu za mawasiliano kama vile masafa ya mawasiliano, nambari za mawasiliano, kikoa cha taifa cha .tz, kanzidata ya anwani na postikodi.

Vilevile, wamejifunza kuhusu uboreshaji wa utoaji wa leseni za mawasiliano, ambazo sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao kupitia jukwaa la Tanzanite, hivyo kuondoa ulazima wa waombaji kufika ofisini.

Wabunge hao wameipongeza TCRA kwa kazi nzuri na ubunifu.