Kufuatia uamuzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwafukuza waandishi na watumishi wengine wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwenye uzinduzi wa kampeni za chama hicho, baadhi ya waandishi wa habari wameazimia kutoandika habari zinazohusu chama hicho.
Umoja wa Waandishi wa Habari wa Kujitegemea Kanda ya Pwani (UWHP) ni miongoni mwa waliochukua uamuzi huo na kusema kuwa kitendo kilichofanywa na CHADEMA mbali na kukiuka mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia, pia kimewanyima wananchi fursa ya kupata sera zilizotolewa na chama hicho katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu.
“Umoja wa Waandishi wa Kujitegemea Kanda ya Pwani tunatamka rasmi kuwa hatutachapisha taarifa zinazohusu CHADEMA mpaka watakapoomba radhi kwa TBC na wananchi,” imeeleza taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa UWHP, Abdallah Nassoro.
Mbali na hilo, UWHP imetoa rai kwa vyombo vya habari na klabu za waandishi nchini kutochapisha taarifa zinazoihusu CHADEMA.
Agosti 28, 2020 kwenye uzinduzi wa kampeni za CHADEMA, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alitoa dakika 15 kwa watumishi wa TBC kuondoka kwenye uwanja wa Mbagala-Zakhiem kwa madai kuwa wamekata matangazo mbashara wakati alipoanza kuzungumza. Hata hivyo madai hayo hayakuwa ya kweli kwani hadi anatoa agizo hilo, matangazo yalikuwa hewani.