Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amewasihi waandishi wa habari nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuepuka makosa ya kisheria yanayoweza kujitokeza.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akitoa mada wakati wa mafunzo kwa Waandishi wa habari za mtandaoni wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) – TBCOnline.
Amewataka waandishi wa habari za mtandaoni kutojiona wanyonge kwa kufanya kazi hiyo, bali wajione watu waliobeba dhamana kubwa katika kuihabarisha jamii mambo mbalimbali yanayoendelea duniani.
Si lazima Waandishi wote wa habari waonekane kwenye televisheni, kuna namna nyingi za kufanya kazi hii ikiwemo mitandao ya kijamii ambayo watumiaji wake wanaongezeka kwa kasi, kwa sasa “Dunia imehama kutoka mtaani kwenda mtandaoni.” amesema Dkt. Abbasi.