Vyuo vikuu tisa vyaruhusiwa kudahili wanafunzi baada ya kurekebisha kasoro

0
490

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesema katika kusimamia ubora wa elimu inayotolewa na vyuo vikuu nchini, kati ya kipindi cha mwezi Oktoba 2016 hadi Januari 2017, ilifanya ukaguzi maalum wa kitaaluma kwa taasisi 64 za vyuo vikuu, vyuo vikuu vishiriki na vituo vya vyuo vikuu ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Katibu Mkuu wa TCU, Prof. Charles Kihampa amesema kuwa katika uchunguzi huko walibaini kasoro na kuchukua hatua ili kuhakikisha kuwa utoaji wa elimu unakuwa wa kiwango kinachokubalika.

‘’Matokeo ya ukaguzi yalibainisha kasoro mbalimbali katika uendeshaji wa vyuo vikuu nchini, vyuo 45 vilikutwa na kasoro ndogondogo, vilipewa ushauri na viliweza kurekebisha katika kipindi kifupi vikaendelea na utoaji wa elimu ya juu na vyuo 19 vilikutwa na kasoro kubwa, vilipewa ushauri na muda wa mrekebisho.’’

Kwa mujibu wa Prof. Kihampa hadi sasa vyuo vikuu tisa kati ya 19 vilivyositishwa udahili vimefanya marekebisho makubwa na vimeruhusiwa kudahili na kuendelea kutoa mafunzo kwa baadhi ya programu za masomo, na kuvitaja vyuo hivyo kuwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Umoja wa Afrika Tanzania (UAUT), Chuo Kikuu cha Teofila Kisanji (TEKU), Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora (AMUCTA), Chuo Kikuu Kishirishi cha Marian (MARUCo).

Vyuo vingine ni Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala Nchini Tanzania (KIUT), Chuo Kikuu Kishiriki cha Kikristo cha Tiba Kilimanjaro (KCMUCo), Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stephano- Moshi (SMMUCo) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Mt. Fransisko (SFUCHAS).

Ameongeza kuwa mifumo ya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara imefanya vyuo kufanya maboresho makubwa katika miundombinu ya kufundisha na kujifunzia ikiwa na pamoja na ujenzi wa maabara za kisasa, mifumo ya mawasiliano ya kielektroniki, madarasa na kuongeza idadi ya viongozi na wahadhiri wenye sifa.