Vyombo vya ulinzi na usalama vimeagizwa kuimarisha ulinzi wa mipaka yote nchini, ili kuzuia watu kuingia nchini bila kufanyiwa uchunguzi.
Agizo hilo limetolewa na Rais John Magufuli wakati akihutubia Taifa kueleza hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na serikali katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.
Amesema maeneo ya mipaka ni miongoni mwa maeneo ya hatari yanayoweza kusababisha kuenea kwa virusi vya corona, hivyo ni vema maeneo hayo yakaangaliwa kwa umakini na kuhakikisha hakuna watu wanapita katika maeneo hayo kinyume cha sheria.
Rais Magufuli amewakumbusha Watanzania kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya kuhusu namna ya kujikinga na virusi vya corona.
Amewasihi pia kujiepusha na mikusanyiko isiyo ya lazima, na kwa maeneo ambayo mikusanyiko haiwezi kuepukika kama kwenye hospitali, masoko, maduka, kambi, misikiti, makanisa na kwenye vyombo vya usafiri wa umma, wahusika wanaosimamia maeneo hayo wahakikishe wanachukua tahadhari zote muhimu ili maeneo hayo yasiwe chanzo cha kuenea kwa virusi hivyo.