Vyombo vya habari Oman kuitangaza Tanzania

0
48

Tanzania na Oman zimekubaliana kushirikiana katika sekta ya Mawasiliano, Habari na Teknolojia.

Chini ya makubaliano hayo, nchi hizo zitatumia vyombo vyake vya habari kuhabarisha umma katika masuala mbalimbali ya kijamii, kutangaza tamaduni na kubadilishana ujuzi wa teknolojia.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, alipokutana na waziri wa Habari wa Oman Dkt. Abdullah bin Nasser bin Khalifa Al-Harassi nchini Oman.

Katika mazungumzo hayo Waziri Nape ameeleza kuwa, kutokana na uhusiano wa kihistoria wa muda mrefu kati ya Tanzania na Oman, nchi hizo zinapaswa kuhabarishwa juu ya undugu wa damu kati ya watu wa mataifa hayo ili kuendeleza uhusiano huo.

Kwa mujibu wa Waziri Nape, Oman kupitia vyombo vyake vya habari itaitangaza Tanzania katika mataifa mengine ili kuvutia biashara, uwekezaji na utalii.

Akiwa Oman, waziri huyo wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye pia ametembelea chumba maalum kinachotumika katika shughuli za uandaaji wa habari za magazeti, Redio na Televisheni kwa lengo la kufahamu taratibu za uandaaji wa vipindi nchini humo.