Vyama vya siasa havijazuiliwa kufanya shughuli zake : Waziri Mkuu

0
264

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa vyama vya siasa nchini havijazuliliwa kufanya shughuli zake za kisiasa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Akijibu maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa utaratibu uliopo sasa unaoonekana kama kuvinyima nafasi vyama vya siasa kufanya shughuli zake unalenga kuwawezesha Wanasiasa kufanya shughuli za kisiasa katika maeneo yao pasipo kubughudhiwa na Wanasiasa kutoka nje.

Waziri Mkuu Majaliwa alikua akijibu swali la Papo kwa Papo kutoka kwa Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe ambaye alitaka kufahamu ni lini Serikali itaviruhusu vyama vya siasa kufanya shughuli zake kama ilivyokua miaka ya nyuma.

Kuhusu  suala la kuwepo kwa Tume huru ya Uchaguzi, Waziri Mkuu Majaliwa amesistiza kuwa Tume ya Taifa ya  Uchaguzi iliyopo sasa ni huru kwa kuwa imekua ikitekeleza majukumu yake kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu yeyote awe Kiongozi ama Mwanasiasa.

Aidha Waziri Mkuu amesema kuwa si kweli kwamba nchi inaongozwa kibabe kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, bali inaongozwa kwa kufuata misingi ya Kidemokrasia.