Viwanja vya Nanenane kutoa mafunzo kwa wakulima mwaka mzima

0
351

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka kwa namna alivyoandaa Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Uvuvi (Nanenane) kwa miaka mitatu mfululizo.

Aidha, ameeleza kufurahishwa na uamuzi wa Wizara ya Kilimo wa kufanya eneo la viwanja wa Nyakabindi yanapofanyika maonesho hayo kuwa eneo la kudumu la kutoa mafunzo wa wafugaji, wakulima na wavuvi katika kipindi chote cha mwaka.

Waziri Mkuu amezitaka taasisi ambazo hazijajenga majengo ya kudumu katika viwanja vya Nyakabindi zifanye hivyo ili eneo hilo liwe la kudumu kweli na kuweza kutoa huduma kwa wananchi.

Akizungumzia uamuzi huo, Waziri Luhaga Mpina amesema kuwa wameona hawawezi kuleta mabadiliko katika sekta hizo nyeti zinazogusa idadi kubwa ya Watanzania kwa kutoa mafunzo kwa siku nane tu kwa mwaka, ndio sababu ya kuamua kufanya eneo hilo kuwa la kudumu.

Maonesho ya Nanenane huanyika kila mwaka kuanzia Agosti 1 hadi Agosti 8 ambapo hujikita zaidi katika kutoa elimu/mafunzo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi juu ya namna ya kukuza uzalishaji katika sekta zao.