Viwanda zaidi vyaendelea kujengwa

0
1851

Serikali imesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu zaidi ya viwanda elfu tatu na sitini vimejengwa na hivyo kutoa fursa kwa Watanzania wengi.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Rais John Magufuli wakati wa kongamano la hali ya Uchumi na Siasa nchini lililoandaliwa na Chuo Kikuu Cha Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Rais Magufuli ameongeza kuwa pamoja na serikali kufanya jitihada kubwa za kujenga viwanda vipya, pia ina mpango wa kuvichukua viwanda ilivyovibinafsisha na ambavyo havizalishi kama ilivyotarajiwa.

Kuhusu  hali ya uchumi nchini, Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania ni miongozni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi na kwamba hadi sasa umekua kwa asilimia Saba, huku mfumuko wa bei ukiimarika.

Amesisitiza kuwa nchi ina fedha za kutosha na hadi sasa ina akiba ya dola bilioni 5.4 za Kimarekani, akiba ambayo haijawahi kuwepo toka uhuru na inayoweza kutosheleza kwa muda wa miezi sita.

Rais Magufuli ameahidi serikali yake kuyashughulikia mambo yote yaliyowasilishwa kupitia mada mbalimbali, kwa maana yana mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.

Miongozi mwa watoa mada katika kongamano hilo la hali ya Uchumi na Siasa nchini, lililohudhuriwa na washiriki kutoka sekta mbalimbali ni Profesa Humphrey Mushi, Profesa Rwekaza Mukandala na Profesa Kitila Mkumbo.