Maafisa ustawi wa jamii wa wametakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vituo vya kulea watoto (day care) ili kujiridhisha wakati wote kuwa vinazingatia masharti na kuhakiki kuwepo kwa mazingira salama kwa watoto.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Naftali Ng’ondi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mpango wa ukaguzi wa uendeshaji wa vituo hivyo.
Kwa mujibu wa Dkt. Ng’ondi, kumekuwepo na changamoto za malezi ya watoto katika vituo hivyo ikiwa ni pamoja na vituo kuanzishwa kiholela, kuendeshwa bila kusajiliwa, kutozingatia masharti ya usajili na kuwepo kwa mazingira yasiyo salama kwa watoto.
“Kumekuwa na baadhi ya watu wanaoanzisha vituo hivi bila kufuata sheria zilizowekwa na serikali na wapo ambao wameanzisha vituo hivyo kwenye mazingira ambayo sio salama kwa watoto,” amesema Dkt. Ng’ondi.