Mjadala wa upatikanaji kwa wakati vitambulisho vya uraia maarufu Vitambulisho vya NIDA umeibuka Bungeni wakati wa kipindi cha maswali na majibu, ambapo wabunge wameibana serikali kuhusiana na upatikanaji wa vitambulisho hivyo kwa wananchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Yusuf Masauni amelieleza Bunge kuwa, ucheleweshaji wa vitambulisho hivyo unatokana na changamoto tatu, kubwa zaidi ni changamoto ya kimkataba na upatikanaji wa kadi ghafi katika soko la dunia.
Mhandisi Masauni amesema, kwa sasa changamoto hizo zimemalizika na kwamba serikali imetenge shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kununua kadi ghafi milioni 8.5 kwa ajili ya kutengenezea vitambulisho hivyo.
Awali mbunge wa Viti maalum Faharia Shomari (CCM) alitaka kujua lini serikali itamaliza tatizo la ucheleweshaji wa vitambulisho vya uraia kwa wananchi, na hatua ambazo serikali inachukua kukabiliana na tatizo hilo.