Visimbuzi kuonesha chaneli za ndani bure

0
2482

Serikali imesema kuwa kuanzia Septemba Tano mwaka huu visimbuzi vitaanza kuonesha chaneli zote za ndani bila kutoza gharama yoyote kwa mtazamaji.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu yaliyojadiliwa katika kikao kati ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe na wadau na wamiliki wa televisheni nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi amesema kuwa serikali imefikia uamuzi huo baada ya visimbuzi vya Azam, Zuku na DSTV kutoonesha chaneli za ndani kulingana na aina ya leseni zao.

Dkt Abbasi amesisitiza kuwa kuanzia Septemba Tano mwaka huu visimbuzi vya TIN, Starmedia, Continental na Digtek vitaonesha takribani chaneli 34 za ndani bure ili kutoa fursa ya kila mwananchi kuwa na haki ya kupata taarifa.

Amesema kuwa wadau hao na wamiliki wa televisheni wameonesha kuridhishwa na hatua hiyo ya kwa vile serikali imetengeneza miundombinu itanayoruhusu chaneli zao kuonekana nchi nzima.

Kikao hicho kati ya Waziri Mwakyembe na wadau na wamiliki wa televisheni nchini kimefanyika kwa lengo la kuwa na majadiliano ya pamoja baina serikali na wadau hao ili kupata muafaka kuhusu kutooneshwa kwa chaneli za ndani katika visimbuzi vilivyokiuka masharti ya leseni zao.