Viongozi watakiwa kujaza fomu za maadili kabla ya Desemba 30

0
302

Rais Dkt John Magufuli amemuapisha Jaji Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi kuwa Kamishna wa Maadili.

Akizungumza baada ya kumuapisha na kushuhudia Jaji Mwangesi akila kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, Rais Magufuli amemtaka kwenda kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake Marehemu Jaji Mstaafu Harold Nsekela.

Rais Magufuli amewasisitiza viongozi wote wa umma takribani ELFU 15 wanaotakiwa kujaza fomu za maadili, kufanya hivyo kabla ya Desemba 30 mwaka huu kwa mujibu wa sheria na kwamba ndio maana amemteua, Kamishna wa Maadili, Jaji Mwangesi kujaza nafasi iliyoachwa na Marehemu Nsekela ili kusiwe na visingizio.

Aidha, Rais Magufuli ameitaka Sekretarieti ya Maadili ya viongozi kuachana na ujazaji na uwasilishaji wa fomu za maadili ya uongozi kwa njia ya mtandao ili kuepusha uvujaji wa siri na ubadilishaji wa maudhui ya fomu hizo, na badala yake fomu zichukuliwe mtandaoni na kisha kujazwa na kuwasilishwa nakala halisi kwa ofisi husika.

Hafla ya kuapishwa kwa Jaji Mwangesi kuwa Kamishna wa Maadili imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deo Ndejembi, Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Rufani Kanda ya Dodoma, – Latifa Mansour.

Rais Magufuli pia ametumia hafla hiyo kuwatakia Watanzania wote heri ya sikukuu ya Krismasi pamoja na Mwaka Mpya.