Viongozi waonywa kutoingilia vyama vya ushirika

0
138

Waziri wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda amewaonya baadhi ya viongozi wenye tabia ya kuingialia Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Mazao (AMCOS) huku akiwataka kuacha tabia hiyo mara moja.

Aidha, amesema ushirika sio idara ya serikali hivyo hauwezi kuongozwa kama idara kwa kuwa mamlaka yake ina mipaka na hakuna kiongozi anayetakiwa kuingilia matumizi ya fedha wala kuzipangia matumizi.

”Tumepambana sana na wabadhirifu kwenye ushirika na kurejesha mali mbalimbali zilizoibwa kupitia ushirika hivyo kurudisha imani ya wanaushirika, na mali zao haziwezi kufanyiwa ubadhirifu wa aina yoyote.

Tutaendelea kusimamia ushirika kuhakikisha kwamba unaendelezwa kwa weledi, uwajibikaji na uwazi ili watu wengi wakubali kujiunga na ushirika kwa sababu unasaidia sana kunyanyua hali zao za kimaisha kwa kuwa ni hiari kujiunga hakuna kulazimishwa,”alisema.

”Na hili ni muhimu kwa sababu kuna mahali ametokea kiongozi mmoja kaingia kwenye AMCOS anatoa amri toa shilingi milioni 25 hapa peleka kule, hatuna mamlaka hayo, ushirika ni hiyari ya wanaushirika. Hapaswi kupelekesha wana ushirika wanapaswa kujisikia kwamba ushirika ni mali yao, wasimame kidete, wasimamie shughuli zao bila kuingiliwa kinyume na taratibu zinazokubalika,” amesema.

Alisisitiza anasema hilo kwa sababu kuanzia Waziri wa kilimo (yeye), Mrajisi wa ushirika, wote lazima wajue mpaka upi wa kwao au si wao.