Viongozi waliotumia vibaya fedha za TASAF watakiwa kuzirejesha

0
239

Rais John Magufuli amewataka viongozi wote wa Serikali waliochukua fedha za mpango wa kunusuru kaya maskini nchini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kuzitumia isivyo sahihi kuzirejesha mara moja.

Akizungumza jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa kipindi cha Pili cha awamu ya Tatu ya mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na TASAF, Rais Magufuli amesema kuwa serikali haipo tayari kuona fedha hizo zikitumika kinyume na malengo yaliyokusudiwa, hivyo ni lazima zirejeshwe haraka.

Rais Magufuli amefafanua kuwa katika uhakiki uliofanyika, Serikali imebaini changamoto mbalimbali katika mfuko huo ikiwemo malipo kwa kaya hewa nchini.

Ametolea mfano uhakiki uliofanyika kuanzia mwezi Novemba mwaka 2015 hadi mwezi Juni  mwaka 2017 ambapo ilibainika uwepo wa kaya hewa zaidi ya elfu 73 ambapo kaya  zaidi ya Elfu 22 zilithibitika kuwa wanakaya wake si masikini, kaya Elfu 18 na 700 ambazo hazikujitokeza mara mbili kupokea ruzuku na kaya  zaidi ya 990 zilizohamia vijiji, mtaa ama shehia ambako mpango haujaanza.

‘’Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, -Paul Makonda naye pia anasema aliwahi kunufaika na TASAF na alisema alizitumia katika safari yake ya kwenda Dodoma katika masuala yake, sasa naomba fedha hizo uzirudishe mara moja kama ulizitumia katika matumizi hayo uliyoyasema’’, ameagiza Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amezitaja halmashauri Kumi zilizoathirika zaidi na kaya hewa kuwa ni Songea Manispaa mkoani Ruvuma, Chamwino mkoani Dodoma, Kinondoni  na Ilala mkoani Dar es salaam, Moshi Manispaa  mkoani Kilimanjaro, Arusha Mjini, Temeke  mkoani Dar es salaam, Dodoma Mjini, Buhigwe  mkoani Kigoma pamoja na Morogoro na kuongeza kuwa hiyo ni aibu kwa viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri hizo.