Waziri Mkuu Mstaafu David Cleopa Msuya, amewataka viongozi na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mwanga kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuufanya mji wa Mwanga kuwa na hadhi inayostahili.
Waziri Mkuu Mstaafu Msuya ameyasema hayo wilayani Mwanga wakati akifungua mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mwanga.
Amesema yapo maeneo yana miradi ambayo imekuwa ikijengwa kwa kasi ndogo hali inayodidimiza maendeleo ya wilaya hiyo.
“Madiwani wapo, vijiji vipo tumeshindwa, na unaweza kuzunguka wiki moja hadi wiki mbili yapo mambo yanatisha.” amesema Waziri Mkuu mstaafu David Msuya
Amesema lengo la wana Mwanga ni kuona viongozi wanatoka walipo kwa kuwaletea maendeleo kwani haitapendeza kuona viongozi wapo lakini hakuna maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi amewataka wana CCM kuanzia ngazi ya chini kufuatilia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao kujua thamani ya miradi na utekelezaji wake
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha miezi sita, Mbunge wa Jimbo la Mwanga Anania Tadayo amesema kila kata imeweza kupata miradi ya maendeleo ambapo kiasi cha shilingi Bilioni 4.5 inatumika katika kutekeleza miradi hiyo.