Viongozi wa vyama vya Ushirika waonywa

0
250

Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa amesema kuwa, serikali itawachukulia hatua  za kisheria viongozi wa Vyama vya Ushirika ambao wamekua wakitumia vibaya madaraka yao kwa kufanya ubadhirifu wa fedha za Wakulima.

Waziri Bashungwa ametoa kauli hiyo wilayani Karagwe mkoani Kagera, wakati wa maadhimisho ya miaka Ishirini na Mitano ya shirika lisilo la Kiserikali la Mavuno, shirika ambalo limekua likiwasaidia Wakazi wa wilaya hiyo kupitia sekta za Kilimo pamoja na Elimu.

Waziri Bashungwa pia amesema kuwa, serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za shirika hilo katika kuendeleza rasilimali zilizopo wilayani humo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo lisilo la Kiserikali la Mavuno, – Charles Bahati amesema kuwa, wanakabiliana na changamoto mbalimbali wakati wa kutekeleza majukumu yao wilayani Karagwe ikiwa pamoja na tabia ya baadhi ya familia wilayani humo ya kukatisha masomo kwa watoto wao wa  kike ili wakafanye kazi za nyumbani kwenye maeneo ya mijini.

Shirika hilo linatoa huduma za ugani katika sekta ya kilimo, elimu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na huduma nyingine za kijamii kama maji katika vijiji vya Ihanda, Lukole na Chonyonyo  kwenye wilaya hiyo ya Karagwe.