Wanawake Viongozi kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini wametakiwa kuwa na kauli moja katika kutafuta usawa wa kijinsia kwenye masuala ya kiuongozi na kisiasa, ili kuongeza idadi ya Wanawake wanaoitumikia jamii.
Kauli hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na Mratibu wa Asasi ya Ulingo Dkt. Avemaria Semakafu, wakati akifungua warsha ya viongozi Wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini, warsha iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
“Tukae tujadiliane kama tunaridhika na mustakabali wa Wanawake ndani ya uongozi wa kisiasa, kuangalia ndani ya vyama vya siasa kama tunaridhika na nini kifanyike tuweze kutoka na kujua tutawajibikaje kuona tunatoka, maana naweza kusema sisi ndio wasimamizi wa nchi.” amesisitiza Dkt. Semakafu
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi amesema Wanawake wanatakiwa kuwa wamoja ili waweze kufika mbali katika masuala ya uongozi.
“Sisi lazima tujiulize ni juhudi gani tunazifanya kuhakikisha vijana wanaokuwa nao wanapata nafasi za uongozi ili kuondoa tabaka la uongozi kwa vizazi vijavyo.” ameongeza Liundi
Nao baadhi ya washiriki wa warsha hiyo akiwemo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania, (UWT) mkoa wa Dar es Salaam, Grace Haule na Aisha Machano ambaye ni Mwenezi wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) Taifa wamesema, warsha kama hizo zinawasaidia Wanawake kujadili na kuelekezana mambo ya uongozi pamoja na kuwaimarisha katika utekelezaji wa majukumu yao wanapopata nafasi za uongozi.