Imeelezwa kuwa viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika kuwaelimisha waumini wao kuhusu majanga yanayotokea ndani ya jamii likiwemo la UVIKO-19 ambalo bado ni tishio duniani.
Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Mbeya wamekuwa na maoni tofauti juu ya utoaji elimu ya ugonjwa wa UVIKO-19 katika mkoa huo, unaotajwa kuwa na madhehebu mengi ya dini nchini ikilinganishwa na mikoa mingine.
Miongoni mwa wakazi hao ni Omary Abdallah ambaye amesema viongozi wa dini wanapaswa kuwaelimisha waumini wao juu ya umuhimu wa kuyasoma na kuyaelewa mafundisho yaliyomo kwenye vitabu vya dini.
Amesema vitabu vya dini pia vinasisitiza kulinda afya ya mwanadamu na kuongeza kuwa mtu kupata chanjo ni sehemu ya kutimiza maandiko ya vitabu hivyo.
Naye Maria Frank amewakumbusha viongozi wa dini kusaidiana na serikali katika kuwasisitiza waumini wao kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO -19.
Kadhi wa mkoa wa Mbeya, Hassan Mbarazi amesema mafunzo kuhusu afya ya akili na msaada wa kisaikolojia yanayoendelea kutolewa mkoani Mbeya kwa maafisa ustawi wa jamii, wahudumu wa afya na azaki zinazotoa huduma ya afya ya jamii kuwajengea uwezo wa kutoa huduma za afya ya akili na saiokolojia kwa jamii yaliyofadhiliwa na Amref na kuratibiwa na PHEDES Tanzania yatasaidia kuwakumbusha viongozi wa dini kutimiza wajibu wao wa kuhamasisha waumini wao kujitokeza kupata chanjo dhidi ya UVIKO -19.
Kwa upande wake Subisya Kabuje kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wanaotoa elimu kwa jamii kuhusu uelewa wa umuhimu wa kupata chanjo mbalimbali ikiwemo ya UVIKO -19.
Ameongeza kuwa kuwepo kwa mafunzo hayo kutasaidia watoa huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kuimarika na kufikia lengo la kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa wananchi kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19.
Taasisi ya PHEDES Tanzania kwa kushirikana na Amref wanaendesha mafunzo ya siku tano mkoani Mbeya kwa maafisa ustawi wa jamii, wahudumu wa afya na azaki zinazotoa huduma za afya ya jamii ili kuwajengea uelewa wa kutoa huduma za afya ya akili na saiokolojia kwa jamii.