Viongozi wa Afrika wapewa somo

0
2388

Viongozi wa Bara la Afrika  wametakiwa kuhakikisha chaguzi mbalimbali zinazofanyika katika mataifa yao zinafanyika kwa kuzingatia kanuni na sheria.

Wito huo umetolewa jijini Dar es salaam na baadhi ya wasomi na wanasiasa wakati wa mdahalo wa wazi wa kumbukizi ya  miaka 19 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambapo miongoni mwa mada zilizojadiliwa ni ile inayohusu mienendo ya chaguzi na mustakabali wa mataifa ya Afrika.

Akifungua mdahalo huo, Mwenyekiti wa Kigoda  cha Mwalimu Nyerere, Profesa Rwekaza Mukandala amesema kuwa nchi nyingi za Bara la  Afrika  zimekuwa zikifanya chaguzi ambazo hazileti tija katika mataifa yao bali kuchochea migogoro ya kisiasa.

Amesema kuwa jambo kubwa ambalo mataifa ya Afrika  yanatakiwa kufahamu ni kuendeleza  yale yaliyoasisiwa na waasisi wa mataifa hayo ambao walikuwa na mwelekeo wa kuimarisha  demokrasia iliyoleta tija ndani ya mataifa yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu  Nyerere, -Joseph Butiku  amesema kuwa Watanzania wanatakiwa  kufahamu kuwa amani ni jambo la kuzingatiwa katika kipindi cha uchaguzi ili taifa liendelee kuwa na amani na utulivu.