Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika vijiji vyote nchini vikiwemo vile vya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo mkoani Kagera mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji wa Kemondo – Maruku ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema kwa sasa Serikali inaendelea kutekeleza kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani, kampeni yenye lengo la kuhakikisha huduma ya maji inapatikana katika maeneo ya karibu na kuwawezesha Wanawake hasa wa maeneo ya vijijini wamapata muda wa kushiriki katika shughuli za kijamii.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti yenye lengo la kumaliza tatizo la maji nchini, hivyo Wananchi waendelee kuwa wavumilivu wakati mikakati hiyo inatekelezwa.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) wilaya ya Bukoba, Mhandisi Evaristo Mgaya amesema mradi huo wa maji wa Kemondo – Maruku unalenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika kata tano za wilaya ya Bukoba na moja ya wilaya ya Muleba.
Amesema vijiji vinakavyonufaika na mradi huo ni vya kata za Kemondo, Maruku, Nyangereko, Bujugo na Katerero wilayani Bukoba na kata ya Muhutwe wilayani Muleba.
Mradi huo unatekelezwa kwa awamu na unakadiriwa kunufaisha Wananchi 117,461 kwa gharama ya shilingi bilioni 15.9.