Naibu Waziri wa Tawala la Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwita Waitara, amewataka vijana kujikita kikamilifu katika shughuli za kilimo.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya Nanenane mkoani Simiyu amesema asilimia kubwa ya vijana huhofia mikopo kutokana na hofu ya matokeo ya kushindwa kulipa mkopo huo, huku akitaja watu wazima pia kuwa na hofu hiyo.
Naibu waziri huyo wa TAMISEMI amesema hayo wakati akihotubia katika hafla iliyoandaliwa na mikoa ya Kanda ya Ziwa Mashariki kwa ajili ya kuhamasisha vijana kufanya shughuli za kilimo.
Aidha, ameziomba benki zilizosaidia kuratibu shughuli hiyo kusaidia vijana waelewe vyema masharti ya mikopo na namna wanavyoweza kuitumia kwa manufaa ya jamii.
Ambao hawakuachwa nyuma ni viongozi wa halmashauri kwani wao wameombwa kupitia wananchi wa halmashauri zao na kujionea kazi hizi kubwa wanazozifanya wananchi wao bila kusubiri Nanenane.
Walioongozana na Waitara katika ziara hiyo ni Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Karolina Mtaphula na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Miriam Mmbaga.