Vijana 80 huambukizwa UKIMWI kila siku nchini

0
313

Kamati ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI imeeleza kwamba vijana 80 huambukizwa Virusi vya UKIMWI kwa siku, kwa mwezi ni vijana 2400, sawa na maambukizi 28,800 kwa mwaka.

Kamati imetoa takwimu hizo wakati ikiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wanachangia maambukizi kwa asilimia 40 ya maambukizi yote kitaifa, ambapo kiwango cha maambukizi kwa wasichana asilimia 2.1 na wavulana ni asilimia 0.6.

Sababu kubwa zinazochangia kuongezeka kwa maambukizi mapya kwa wasichana rika balehe ni kuanza ngono wakiwa na umri chini ya miaka 15 na wavulana asilimia 14.3 hufanya ngono na watu wasio rasmi.

Ili kukabiliana na janga hilo, Kamati imeishauri Serikali kuendelea kushirikiana na wadau, wazazi na walezi kutoa mafunzo ya malezi bora ya afya ya uzazi kwa vijana walioko shuleni na nje ya shule na hatua za mabadiliko ya tabia.