Vifaa vya kunyanyua mizigo kwenye mradi wa JN HPP vyazinduliwa

0
232

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amezindua rasmi vifaa vya kunyanyulia makontena ya mizigo na vifaa vizito vitakavyotumika kwenye utekelezaji wa mradi kufua umeme wa Julius Nyerere Hydro Power Project (JN HPP) katika mto Rufiji.

Akizungumza katika stesheni ya Fuga, Mhandisi Nditiye amesema kuwa serikali imenunua vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na vile vyenye uwezo wa kunyanyua Tani 45, vyenye uwezo wa kunyanyua Tani 15 na  vingine vyenye uwezo wa kunyanyua  Tani Tano kwa gharama ya Shilingi Bilioni Tatu Nukta Tano.

“Vifaa hivi vimenunuliwa na serikali ili kuiwezesha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kutekeleza majukumu iliyopewa ya upokeaji makontena ya mizigo ya ujenzi wa bwawa la kufua umeme la JN HPP katika mto Rufiji, mradi utakozalisha Megawati 2,115 na kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa viwanda”, amesema Naibu  Waziri Nditiye.

Ameongeza kuwa, serikali itaendelea kuiwezesha TAZARA ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kwenye utekelezaji wa mradi huo wa kufua umeme katika mto Rufiji.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt Hassan Abbasi amesema kuwa, serikali inaiboresha stesheni ya kupokea na kushushia mizigo ya Fuga ambayo  itasaidia ujenzi wa mradi huo kufanyika  kwa haraka zaidi.

“Tunatekeleza uboreshaji huu wa stesheni ya Fuga, tumeleta mitambo ya kisasa mikubwa kabisa ambayo imedhaminiwa na serikali kwa ajili ya kuhudumia ujenzi wa bwawa la kufua umeme, kwa hiyo mitambo hii imefika, inafanya kazi na inasambazwa na kampuni ya kizawa”, amesema Dkt Abbasi.